Mwenyekiti wa Taasisi ya Mbeya Family Group (MFG), Michael Mwangoka, ametoa wito kwa wananchi wa Mbeya kuhakikisha wanatunza miti na mazingira ya mji huo ili kurejesha hadhi yake ya zamani kama “Green City.”
Akizungumza wakati wa zoezi la kupanda miti lililofanyika eneo la Majengo jijini Mbeya, Mwangoka alisisitiza umuhimu wa kuhifadhi mazingira kwa faida ya vizazi vijavyo. Aliwataka wananchi kuendelea kushirikiana katika juhudi za kutunza miti na kuhakikisha kuwa mji wa Mbeya unarejea kuwa mfano wa miji yenye mandhari ya kijani na mazingira safi.
Mwangoka aliwashukuru wanachama wa Mbeya Family Group pamoja na wadau wengine walioshiriki katika shughuli hiyo muhimu ya kupanda miti, akibainisha kuwa hatua hiyo ni moja ya mikakati ya kukabiliana na changamoto za kimazingira zinazoikumba dunia kwa sasa.