Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mbeya (Mbeya UWSA), kupitia Mwenyekiti wa Bodi yake, Bi. Edna Mwaigomole, imekabidhi tenki la maji lenye ujazo wa lita 5,000 kwa Shule ya Sekondari ya Wanawake Tulia, iliyopo Iyunga, Jijini Mbeya.
Hatua hii imekuja baada ya shule hiyo kuwasilisha ombi la msaada wa maji, na mamlaka hiyo kusikia kilio chao. Utoaji wa tenki hilo unalenga kuboresha upatikanaji wa maji safi shuleni hapo, hivyo kusaidia mazingira bora ya kujifunza kwa wanafunzi.
Akizungumza wakati wa makabidhiano, Bi. Mwaigomole alisisitiza dhamira ya Mbeya UWSA ya kuendelea kushirikiana na jamii katika kuhakikisha huduma bora za maji zinapatikana kwa taasisi mbalimbali, hususan shule.
Uongozi wa shule hiyo umeishukuru Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mbeya kwa msaada huo muhimu, wakibainisha kuwa utapunguza changamoto ya maji na kuboresha afya na ustawi wa wanafunzi.