Mbeya, Tanzania – Aprili 2025
Wakazi wa maeneo ya Mwansekwa na Igodima jijini Mbeya wameeleza furaha yao kufuatia kuboreshwa kwa huduma ya upatikanaji wa maji safi katika maeneo yao, hali ambayo ni tofauti na ilivyokuwa hapo awali.
Wananchi hao wameipongeza Serikali pamoja na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mbeya (MBEYA-UWSA) kwa juhudi walizozifanya kuhakikisha wanapata huduma ya maji kwa uhakika. Wamesema kuwa huduma hiyo imeleta unafuu mkubwa katika maisha yao ya kila siku, hasa kwa upande wa wanawake na watoto waliokuwa wakitembea umbali mrefu kutafuta maji.
“Kwa sasa tunapata maji karibu kabisa na nyumbani, tofauti na zamani tulipokuwa tukiteseka,” alisema mmoja wa wakazi wa Mwansekwa.
Kwa upande wake, MBEYA-UWSA imeeleza kuwa maboresho hayo ni sehemu ya mpango wa Serikali ya Awamu ya Sita wa kuboresha huduma za maji mijini na vijijini kwa kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma hiyo muhimu kwa maendeleo na ustawi wa jamii.