Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye pia ni Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) na Mbunge wa Mbeya Mjini, Mhe. Dkt. Tulia Ackson, leo tarehe 18 Aprili 2025, ameongoza wananchi wa Jiji la Mbeya katika zoezi la upimaji na matibabu ya macho.
Zoezi hilo limeanza rasmi leo katika Shule ya Msingi Kagera, iliyopo Kata ya Ilomba na litadumu kwa siku tatu mfululizo. Huduma hiyo ya afya ya macho inatolewa bila malipo kupitia Taasisi ya Tulia Trust kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa afya.
Katika hotuba yake, Dkt. Tulia amewasihi wananchi wa Mbeya kujitokeza kwa wingi ili kunufaika na huduma hizo muhimu kwa afya zao, akisisitiza dhamira ya Taasisi ya Tulia Trust katika kuboresha ustawi wa jamii kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo.