Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya imepata tuzo ya pongezi kwa kutambuliwa kwa juhudi zake katika utoaji wa mafunzo katika vituo vya kutolea huduma za afya vya ngazi ya msingi (PHC) Mkoa wa Mbeya kwa mwaka 2024. Tuzo hii imetolewa na Kamati ya Usimamizi wa Huduma za Afya Mkoa (RHMT) ya Mbeya, wakati wa kikaoa kazi cha robo ya mwaka kilichojadili changamoto za vifo vinavyotokana na afya ya uzazi na watoto wachanga kilichofanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali.
Akikabidhi tuzo hiyo, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya na Mganga Mkuu wa Mkoa, Dkt. Elizabeth Nyema, ameeleza wazi kutambua mchango mkubwa wa Hospitali ya Kanda Mbeya katika kuboresha huduma za afya ya uzazi na mtoto mchanga na kusisitiza umuhimu wa kuimarisha uhusiano kati ya vituo vya afya na jamii, ili kuimarisha imani ya wananchi katika huduma zinazotolewa.
Nae Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya, Dkt. Abdallah Mmbaga, akipokea tuzo hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya, Dkt. Godlove Mbwanji, amewashukuru Viongozi na wahusika wote wa kamati hiyo kwa kutambua juhudi za Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya na kutoa rai kwa wadau kuendelea kushirikiana ili kuhakikisha huduma za afya ya uzazi zinapatikana kwa ubora wa hali ya juu kwa kila mwananchi lengo kuu ikiwa ni kuboresha utoa huduma za afya kwa jamii na kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika.