Maadhimisho ya Siku ya Msichana katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, Ndaki ya Mbeya, yalifanyika kwa mafanikio tarehe 10 Mei 2025. Hafla hii ilihudhuriwa na Mgeni Rasmi Mheshimiwa Maryprisca Mahundi, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mbeya na Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Maryprisca Women Empowerment Foundation (MWEF).
Katika hotuba yake, Mh. Mahundi aliwasihi wasichana wa chuo kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuathiri mustakabali wao, akisisitiza umuhimu wa elimu kama nyenzo ya kujikomboa kiuchumi na kijamii. Rasi wa Ndaki ya Mbeya, Prof. Henry Mollel, alishiriki pia na kupongeza waandaaji, akisisitiza umuhimu wa kuendeleza maadhimisho haya kila mwaka.
Hafla hiyo ilijumuisha vipindi vya elimu, burudani, na majadiliano kuhusu nafasi ya msichana katika jamii. Mh. Mahundi aliahidi kuchangia shilingi milioni 5 kwa ajili ya ujenzi wa hosteli ya wanafunzi wa kike Ndaki ya Mbeya.
Siku hii huadhimishwa kila mwaka na Jumuiya ya Wasichana wa Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Mbeya kwa kushirikiana na Serikali ya Wanafunzi (MUSO).