Mkazi wa eneo la Soweto, jijini Mbeya, Rashidi Mkwinda, ambaye ni mwandishi wa habari wa Mbeya Yetu Online TV, amesimulia tukio la kuvamiwa na kupigwa kichwani na watu wanaodhaniwa kuwa vibaka majira ya saa sita usiku.
Amesema alikuwa akirejea nyumbani baada ya kudownload faili kwenye kompyuta, ndipo alipofuatwa na watu hao na kushambuliwa wakati akifungua geti la nyumba yake. Katika tukio hilo alipigwa mara kadhaa kichwani, akaanguka chini na kupoteza fahamu kwa muda, kisha kuibiwa simu ya mkononi pamoja na fedha.
Baada ya kupata msaada kutoka kwa majirani, alikimbizwa hospitalini ambako alishonwa majeraha sehemu mbalimbali za mwili na kufanyiwa kipimo cha CT Scan, huku majibu yakitarajiwa kutoka leo.
Mkwinda ametoa wito kwa mamlaka husika kuchukua hatua madhubuti dhidi ya vitendo vya kihalifu vinavyoendelea kushamiri mitaani.

