Wanawake wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Mbeya wameadhimisha Siku ya Wanawake Duniani kwa kutembelea kituo cha kulea watoto wenye mahitaji maalum cha Funguka Foundation kilichopo Mtaa wa Wasai, Kata ya Ilomba, na kukabidhi msaada wa mashine ya kufulia nguo ili kusaidia shughuli za malezi ya watoto wanaolelewa katika kituo hicho.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Kisa Ngoloke alisema waliguswa na juhudi za mama mlezi wa kituo hicho anayewahudumia watoto wenye ulemavu wa akili, viungo na usonji, akieleza kuwa kazi anayofanya ni kubwa na inahitaji moyo wa kujitoa. Alisema waliona ni vyema kufika kituoni hapo ili kushirikiana na watoto hao pamoja na kumpa moyo mlezi huyo, huku wakiamini kuwa msaada walioutoa utasaidia kurahisisha kazi ya kuwahudumia watoto hao.
Kwa upande wake Meneja wa kituo hicho, Nelly Elisha, aliwashukuru wanawake hao kwa msaada huo akisema utasaidia kupunguza changamoto aliyokuwa akikabiliana nayo ya kufua nguo nyingi za watoto, kazi ambayo mara nyingi alikuwa akiifanya mwenyewe. Alisema kituo hicho kinahudumia jumla ya watoto 78 wakiwemo yatima pamoja na wenye ulemavu wa akili, viungo na usonji, ambapo baadhi yao hulala kituoni huku wengine wakiletwa asubuhi na kurudishwa nyumbani jioni.
Naye Afisa Mtendaji wa Kata ya Ilomba, Regina Kichwika, aliishukuru taasisi hiyo kwa msaada huo na kueleza kuwa kituo hicho bado kina mahitaji mbalimbali, hivyo akatoa wito kwa wadau wengine kujitokeza kusaidia ili kuboresha huduma kwa watoto hao.
Aidha, Kichwika aliwataka wazazi kuacha tabia ya kuwaficha watoto wenye ulemavu majumbani, akisisitiza kuwa kuwatoa na kuwaonesha kwenye jamii kunasaidia kupata msaada pamoja na kuhakikisha wanapata haki zao za msingi.


