Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (COSEA SINKALA, MBEYA.CM) Wilaya ya Mbeya vijijini Akimu Sebastian Mwalupindi amemtaka Mbunge wa jimbo la Mbeya vijijini Mhe. Oran Njeza kuendelea kufanya kazi kwa bidii na weledi kwa maslahi ya wananchi badala ya kusikia maneno ya watu juu ya watu wanaojipitisha jimboni kutaka ubunge mwakani 2025 kitendo anachosema ni kinyume na taratibu za CCM.
Mwalupindi amesema hayo wakati akizungumza kwenye mkutano wa Halmashauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Mbeya vijijini uliofanyika katika mji mdogo wa Mbalizi wilayani Mbeya.
Amesema wanaojipitisha kabla ya muda watashughulikiwa kwani kuna vyombo husika vinavyoona kwakuwa Chama Cha Mapinduzi kina kanuni na taratibu zake akisisitiza kuwa kwa sasa Mbunge ni Oran Njeza ambaye anatakiwa kupewa ushirikiano kuendelea kuwatumikia wananchi wake.
Kwa upande wake Mbunge wa jimbo hilo Mhe. Oran Manasse Njeza, ameishukuru Serikali, Chama Cha Mapinduzi, madiwani na viongozi mbalimbali kwa kuendelea kumpa ushirikiano katika kuwawakilisha wananchi akisema matokeo ya kazi nzuri ikiwemo kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa kamati ya bajeti ya bunge ni kwasababu ya maombi yao.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mbeya Mhe. Mwalingo Kisemba amempongeza Mbunge Njeza kwa kuaminiwa kuongoza kamati ya bajeti huku akisikika akisema ni bora kuwa kiongozi wa kamati hiyo nyeti kuliko kuwa Waziri au naibu Waziri wa wizara.
Katika mkutano huo kaimu mkuu wa wilaya amewaasa viongozi hao wa CCM kwenda kujipanga kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za mitaa, vitongoji na vijiji ili kuhakikisha Chama Cha Mapinduzi kinaibukashindi kote Mbeya vijijini kisha uchaguzi mkuu ujao.
NA JOSEA SINKALA, MBEYA.