Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb), amempongeza Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Mhe. Dkt. Tulia Ackson, kwa uongozi wake wa mfano unaoleta mageuzi chanya kupitia Mbeya Tulia Marathon.
Akizungumza Mei 10, 2025 katika Uwanja wa Sokoine, Mbeya, mara baada ya kushiriki mbio fupi za Tulia Marathon, Mhe. Mahundi alisema kuwa mashindano hayo si tu ni burudani ya michezo bali pia ni jukwaa la kugusa maisha ya Watanzania wengi kupitia uboreshaji wa huduma za afya, elimu na kusaidia makundi yenye uhitaji.
“Spika Tulia si kiongozi tu wa kitaifa, bali ni dira ya matumaini kwa jamii. Kupitia Mbeya Tulia Marathon ameonyesha kuwa michezo ni daraja la maendeleo,” alisisitiza Mhe. Mahundi.
Mashindano haya yameendelea kuthibitisha kuwa michezo inaweza kuwa chachu ya mshikamano, afya bora, na maendeleo endelevu kwa taifa.