Mgombea Ubunge wa Jimbo la Uyole kupitia Chama cha Mapinduzi ( CCM) Dkt. Tulia Ackson, amewaomba Wananchi wa Jimbo hilo kumchagua kwa kura nyingi kwa nafasi yake ya Ubunge na kura nyingi kwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa nafasi ya Urais katika Uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025 ili wakaiendeleze kazi nzuri waliyoianza kwa kuboresha sekta mbalimbali za kijamii.
Akizungumza mbele ya Wananchi wa Jimbo la hilo wakati wa ufunguzi rasmi wa kampeni zake leo tarehe 13 Septemba, 2025 katika Uwanja wa Shule ya msingi Hasanga, Dkt. Tulia amesema kuwa katika kuhakikisha azma hiyo inatekelezeka, kwanza kabisa atahakikisha anafanikisha upatikanaji wa Halmashauri ya Uyole ikiwemo ujenzi wa jengo hilo ambayo itawezesha kukimbiza kasi ya maendeleo ya Jimbo hilo.
Sambamba na hayo, amebainisha vipaumbele vyake atakapopata nafasi ya kuwa Mbunge wa Jimbo hilo jipya ni kuhakikisha anaboresha miundombinu ya Barabara zikiwemo Barabara za Mitaa kujengwa kwa Kiwango Cha lami, Ujenzi wa Vivuko na Madaraja Kwenye kata zote pamoja na kuendelea kwa ujenzi wa Barabara ya njia nne Uyole hadi Ifisi inakamilika kwa wakati.
Vipaumbele Vingine ni Kuboreha Miundombinu Katika sekta ya Elimu ikiwemo Ukarabati wa Madarasa na Kupandisha hadhi shule za sekondari Kuwa Kidato cha tano na sita, Kukamilisha Mradi wa Maji wa mto Kiwira ili kuondoa kero ya upatikanaji wa Maji, Kuboresha huduma za Afya na kuondoa kero wanazozipata wakinamama wajawazito wakati wa Kujifungua na Kununua Magari ya Kubebea Wagonjwa.
Katika hatua Nyingine, Dkt .Tulia amesema kuwa atahakikisha Umeme unapatikana katika Mitaa Yote ya Jimbo la Uyole, bila kusahau sekta ya kilimo atahakikisha wakulima Wanapata Pembejeo Kwa Wakati na kwa bei nafuu. Pia ataweka msukumo kwenye Ujenzi wa viwanja vya Maonyesho ya Nanene na Soko la Kimataifa Ndani ya viwanja hivyo, Kuimarisha sekta ya michezo hasa mchezo wa ngumi.
Ufunguzi huo wa Kampeni za jimbo la Uyole zinazokwenda na kaulimbiu ya “Uyole Kazi” ikilenga Kufanya kazi Kwa Maarifa na Nguvu Zaidi zimehudhuriwa na wagombea udiwani wote wa kata 13 pamoja na Baadhi ya wagombea wa nafasi za ubunge Mkoa wa Mbeya.