Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mhe. Jabiri Omari Makame leo tarehe 15/09/2025 amezindua rasmi huduma mkoba za Madaktari Bingwa wa Dkt. Samia mkoani Songwe ikiwa ni juhudi za Serikali ya awamu ya sita chini ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha huduma bora za afya zinawafikia wananchi wote kwa ukamilifu.
Katika hotuba yake, Mhe. Jabiri Makame ameeleza kuwa ujio wa kambi hiyo ya Madaktari Bingwa wa Dkt. Samia ni ishara ya dhamira ya dhati ya Serikali ya kuimarisha huduma za afya mkoani Songwe. Amebainisha kuwa, kuanzia mwaka 2020 hadi 2025, mkoa umepata maendeleo makubwa ikiwa ni pamoja na ongezeko la vituo vya afya kutoka 205 hadi 273, na hospitali kutoka 2 hadi 5, vyote kwa lengo la kuboresha huduma za msingi na za kitaalamu kwa wananchi.
“Serikali imetenga zaidi ya shilingi bilioni 40.6 kwa ajili ya kuboresha miundombinu, ununuzi wa dawa, vifaa, na vitendanishi, pamoja na kuanzisha afua mbalimbali za tiba ikiwemo lishe, kudhibiti malaria, kifua kikuu, na magonjwa ya zinaa na UKIMWI. Kupitia juhudi hizi, upatikanaji wa dawa umeongezeka kwa asilimia 90, hali inayorahisisha upatikanaji wa huduma na kupunguza vifo vya watoto wachanga kutoka 320 mwaka 2022 hadi 146 mwaka 2023, mkoa umepokea watumishi wa sekta ya afya 725 kuanzia mwaka 2021 hadi 2025, ikiwa ni jitihada za kukabiliana na upungufu wa watumishi wa afya, na kufanya huduma kuwa za karibu zaidi kwa wananchi”. – amesema Mhe. Jabiri Makame
Aidha Mhe. Jabiri Makame, ametoa rai kwa viongozi na watendaji wa mkoa kuhakikisha wanatoa ushirikiano wa karibu kwa madaktari ili kuhakikisha huduma zinazotolewa zinafikia viwango vya juu, na wananchi wanafaidika kwa kiwango cha juu. Pia, amewataka wananchi kushirikiana na wataalamu wa afya ili kufanikisha malengo ya afya bora kwa wote.
Naye Bi. Pasclina Andrew Mratibu wa Huduma Mkoba ya Madaktari wa Mama Samia Mkoa wa Songwe kutoka Wizara ya Afya amesema kuwa uwekezaji huu mkubwa wa Serikali katika sekta ya afya ni hatua muhimu katika kuimarisha afya ya wananchi wa Songwe na kuboresha huduma za matibabu, kwani sasa wananchi hawatalazimika kusafiri kwenda mikoa jirani kwa huduma za kibingwa. Hii ni ahadi na matokeo ya moyo wa Serikali wa kuwaletea wananchi maendeleo na ustawi wa afya.
“ujio wa kambi hii ya matibabu unaleta faida kubwa ikiwa ni pamoja na kutoa huduma za tiba za kitaalamu zilizokuwa zinahitaji kusafiriwa hadi mikoa mikubwa kama Dar es Salaam na Mbeya, hivyo kuokoa muda na gharama za wananchi. Pia, kambi hii itaimarisha uwezo wa wataalamu wa afya kwa kuwapa mafunzo na ushauri wa kitaalamu (mentorship), na kusogeza huduma za kibingwa kwa wananchi wa mkoa wa Songwe” – Pasclina
Timu ya madaktari 30 kutoka kada mbalimbali za afya zikiwa ni pamoja Madaktari wa Uzazi na Magonjwa ya wanawake, Madaktari wa Watoto, Madaktari bingwa wa usingizi na ganzi salama, madaaktari wa magonjwa ya ndani, madaktari wa meno, madaktari wa upasuaji na wauguzi Bingwa wanatarajia kutoa huduma mkoba kwa muda wa wiki moja katika halmashauri 5 za mkoa wa Songwe..