Mbeya – Mwenyekiti wa Kongamano na Mgoda wa Kigoda cha Uprofesa cha Mwalimu J.K. Nyerere katika Taaluma za Umajumui wa Afrika, Profesa Alexander Makulilo, amezungumza na waandishi wa habari mkoani Mbeya akitoa mwito kwa Watanzania kushiriki kikamilifu katika maandalizi ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Prof. Makulilo alizungumza leo wakati akitoa taarifa rasmi kuhusu Kongamano la Uchumi Jumuishi kuelekea Dira 2050, ambalo limeandaliwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kupitia Kigoda cha Uprofesa cha Mwalimu J.K. Nyerere kwa kushirikiana na Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP Centre). Kongamano hilo limepangwa kufanyika tarehe 18 Septemba 2025, katika Ukumbi wa Nkrumah Lecture Theatre wa Chuo Kikuu Mzumbe – Ndaki ya Mbeya, kuanzia saa 5:00 asubuhi.
Umuhimu wa Kongamano
Akieleza sababu za kuandaliwa kwa kongamano hilo, Prof. Makulilo amesema uhitaji wake unatokana na mambo makubwa matatu. Kwanza, ni uzinduzi wa Dira 2050 uliofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Julai 2025 jijini Dodoma. Wakati huo, Rais alisisitiza juu ya kuimarishwa kwa mijadala ya kitaifa kuhusu maendeleo na nafasi ya vijana katika kuibeba Tanzania mpya.
“Mheshimiwa Rais alisisitiza kuwa ni lazima mijadala ya maendeleo irejee katika jamii yetu. Vijana ndio nguvu kazi ya taifa letu, na wao ndio wanapaswa kujipanga vyema ili kutimiza malengo ya Dira 2050,” alisema Prof. Makulilo.
Sababu ya pili ni maandalizi ya bajeti ya mwaka wa fedha 2026/27, ambapo utekelezaji wa Dira 2050 utaanza rasmi. Kwa hiyo, kongamano litawajengea wananchi na wadau uwezo wa kutoa mapendekezo yatakayoingizwa kwenye utekelezaji wa mpango huo wa muda mrefu.
Sababu ya tatu ni maandalizi ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2025/26 – 2029/30), ambao utajengwa kwa kuzingatia mafanikio na changamoto zilizojitokeza katika mpango unaomalizika (2020/21 – 2025/26).
Mada Kuu
Kongamano hili litajadili mada nne kuu:
-
Maudhui na Vipaumbele vya Dira 2050.
-
Msingi wa Uchumi Jumuishi kuelekea Dira 2050, kwa kuangazia mafanikio na changamoto za utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano unaomalizika.
-
Nafasi ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP).
-
Uzoefu wa Sekta Binafsi kama kichocheo cha maendeleo endelevu na jumuishi.
Prof. Makulilo alisema kuwa mijadala hii inalenga kuleta uelewa wa pamoja, ushirikiano na mshikamano wa kitaifa katika utekelezaji wa dira hiyo kubwa ya maendeleo.
Washiriki Wakuu
Kongamano litashirikisha wadau mbalimbali kutoka serikalini, sekta binafsi, asasi za kiraia, vyuo vikuu na washirika wa maendeleo. Baadhi ya watoa mada wakuu watakuwa:
-
Dkt. Fred Msemwa, Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango.
-
Ndugu David Kafulila, Mkurugenzi Mtendaji wa PPP Centre.
-
Dkt. Gladness Salema, Mbunge katika Bunge la Afrika Mashariki.
-
Dkt. Mwajuma Hamza, Mtendaji Mkuu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Wanawake Tanzania.
-
Prof. Humphrey Moshi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
-
Dkt. Jasinta Kahyoza, Chuo Kikuu Mzumbe.
Mwito kwa Wananchi
Akihitimisha mkutano wake na waandishi wa habari, Prof. Makulilo ametoa mwito kwa wananchi na wadau wote kushiriki kikamilifu katika kongamano hilo, ama kwa kufika Mbeya au kupitia vyombo vya habari.
“Kongamano hili ni la kitaifa. Tunawaalika wananchi wote na wadau kutoka sekta mbalimbali kushiriki nasi, kujifunza na kutoa maoni. Taarifa zitakuwa zikifikishwa mubashara kupitia ITV, na kupitia YouTube za Jambo TV na Global TV,” alisema.
Kwa mujibu wake, kongamano hili ni sehemu ya kuandaa taifa kuelekea safari ya kujenga Tanzania jumuishi, shirikishi na endelevu ifikapo mwaka 2050.