Mgombea ubunge wa Jimbo la Uyole kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Ipyana Samson Njiku, ameendelea na kampeni zake za mguu kwa mguu kwa wananchi wa Jimbo la Uyole, ambapo leo ametembelea maeneo ya Kata ya Itezi na Igawilo akiwahamasisha wananchi kujiandaa kwa mabadiliko chanya kupitia uongozi makini na wenye dira ya maendeleo.
Akizungumza na wananchi katika maeneo mbalimbali , Njiku amesema kuwa endapo atapata ridhaa ya wananchi wa Uyole, ataweka kipaumbele katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo:
Ujenzi wa Soko la Kisasa na Kimataifa litakalowezesha wakulima na wafanyabiashara kuuza mazao yao ndani na nje ya nchi kwa urahisi, kuongeza ajira na kipato cha wananchi.
Mradi wa maji kutoka Ziwa Nyasa hadi Jimbo la Uyole, ambao utatatua kwa kiwango kikubwa changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama katika kata mbalimbali za jimbo hilo.
Kuisukuma Serikali kuharakisha ujenzi wa Bandari Kavu ya Inyala, ambayo itakuwa kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi katika mkoa wa Mbeya na Nyanda za Juu Kusini kwa ujumla.
Njiku amesisitiza kuwa kampeni zake zinajikita katika kuwasikiliza wananchi, kuelewa changamoto zao, na kuweka mikakati ya pamoja ya kuzitatua. Amesema chama cha CHAUMMA kinalenga siasa za maendeleo na uwajibikaji, si za maneno bali matendo.