Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya imeanza rasmi kutoa mafunzo ya magonjwa ya Dharura na Mahututi kwa watoa huduma za afya, wanafunzi wa kada za Afya pamoja Jamii Nyanda za Juu Kusini kwa lengo la kuokoa maisha na kupunguza athari za ajali na dharura za kiafya.
Akiongea wakati wa kufungua mafunzo hayo leo tarehe 26 novemba,2025 katika kituo cha kutolea mafunzo hayo kwa vitendo kilichojengwa chini ya udhamini wa taasisi ya Abbott Fund, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya Dkt. Godlove Mbwanji amesema, kuanzishwa kwa mafunzo hayo kutasaidia upatikanaji wa wataalamu wenye weredi kwani kumekuwa na ongezeko la wanafunzi wengi kuliko miundo mbinu ya kufundishia mafunzo haya kwa vitendo.
“…wote tunajua kwamba miaka ya karibuni kumekuwa na ongezeko la wanafunzi kwenye vyuo vyetu ambalo haliendi sambamba na miundombinu ya kufundishia kwa vitendo.” – Dkt. Mbwanji
Aidha Dkt. Mbwanji ameishukuru taasisi ya Abbott Fund Tanzania, Wizara ya Afya pamoja (EMAT) kwa ushirikiano katika ujenzi wa kituo hicho cha kutolea mafunzo hayo.
“…lilianza kama wazo na sasa linaonekana hivyo niwashukuru sana Abbott Fund Tanzania, Wizara ya afya pamoja na (EMAT) kwa kuratibu upatikanaji wa kituo hiki”. – Dkt. Mbwanji
Kwa upande wake Dkt. Raya Mussa, Meneja Mradi huduma za dharura akiongea kwa niaba ya Taasisi ya Abbott Fund Tanzania ameishukuru Wizara ya Afya kupitia Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya kwa ushirikiano waliouonyesha kwa kukubali ujenzi wa kituo ambacho kitawanufaisha watoa huduma za afya, wanafunzi pamoja wataalamu wote wanapatikana Kanda ya Nyanda za Juu Kusini katika idara za Magonjwa ya Dharura na Ajali kutokana na miundombinu pamoja na vifaa ya kisasa vinavyopatikana katika kituo hicho.
“…lengo la kituo hiki si kunufaisha watu wa ndani tu lakini pia itanufaisha wanafunzi pamoja na watu wengine watakaohitaji kujifunza mafunzo haya hata kama si watoa huduma za afya”. – Dkt. Raya Mussa
Dkt. Prosper Bashaka ni Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Dharura na Ajali kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya amesema, maboresho ya upatikanaji wa huduma za dharura imekuwa ni kipaumbele kikubwa cha serikali, hivyo amewapongeza wadau wote walioshiriki katika jitihada za uanzishwaji wa kituo hicho cha kutolea mafunzo ya Magonjwa ya Dharura na Mahututi kwani kitaleta tija kwa hospitali na jamii hasa kwa wakazi wa Nyanda za Juu Kusini.
“…nitoe pongezi kwa wadau wote walioshiriki katika ujenzi wa kituo hiki kwani kitaleta tija kwa hospitali na zaidi wakazi wa Nyanda za Juu Kusini”. – Dkt. Prosper Bashaka.
Hadi sasa vituo hivyo vya kutolea mafunzo ya Magonjwa ya Dharura na Mahututi vimejengwa zaidi ya 6 nchi nzima kwa ushirikiano wa taasisi ya Abott Fund, Wizara ya Afya pamoja na EMART.

