Serikali imeendelea kuanzisha Majukwaa ya Uwezeshaji
Wanawake Kiuchumi kuanzia ngazi ya Vijiji/Mtaa, Kata, Wilaya na Mkoa ambapo Katika kipindi cha mwaka 2020 hadi 2025, jumla ya Majukwaa 15,147 yameanzishwa, ambayo yameleta chachu kwa wanawake ya kujifunza masuala ya ujasiriamali, elimu ya fedha na uwekezaji.
Hayo yamesemwa na Naibu wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mhandisi MaryPrisca Mahundi wakati akizungumza na wanavikundi vya malezi na
matunzo ya watoto Kata ya lhumwa Jijini Dodoma.
Mahundi amesema katika eneo la fursa za kiuchumi, Wizara inaratibu na kusimamia jukumu la kuwezesha kiuchumi wafanyabiashara ndogondogo na wao wakiwa miongoni mwao
watatambuliwa na kuwasajili na kutoa mikopo yenye masharti
nafuu, katika zoezi linalosimamiwa na Maafisa Maendeleo ya
Jamii, Maafisa TEHAMA pamoja na Maafisa Biashara ngazi ya
Mikoa na Halmashauri.
“Tangu zoezi hili lilipoanza mwezi Februari, 2024 hadi kufikia tarehe 26 Novemba, 2025 jumla ya wafanyabiashara ndogondogo 115,035 (Ke 70,894: Me 44,141) wamesajiliwa na jumla ya wafanyabiashara ndogondogo 44,336 waliosajiliwa wamelipia vitambulisho vyao na kwa kutumia vitambulisho hivyo, Benki ya NMB imetoa mikopo ya kiasi cha Shilingi Bilioni 9.8z kwa wafanyabishara hao”. amesema Naibu Waziri Maryprisca
Aidha Naibu Waziri Maryprisca amewapongeza Wadau wa Maendeleo kwa kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali
katika kuimarisha uchumi wa mtu mmoja mmoja na familia sambamba na malezi na matunzo ya watoto katika familia. 
“Nimekuja hapa na wenzangu kushirikishana fursa za kiuchumi kupitia vikundi vyenu lakini pia kuvitumia vikundi hivi kama jukwaa la kukumbushana wajibu wetu wa malezi chanya ya watoto na familia na ni imani yangu mnatambua kuwa familia inajumuisha baba, mama na mtoto au watoto, ingawa kwa mila na tamaduni zetu ndugu na jamaa wa karibu wanaweza kuwa ni sehemu ya familia.
Familia ni chanzo cha jamii yoyote ile Duniani, hivyo ni lazima kuitambua na kuienzi Taasisi hii
muhimu” amesisitiza Naibu Waziri

