
Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkoa wa Dodoma itaendelea kushirikiana kwa karibu na jukwaa la viongozi la uwezeshaji wanawake kiuchumi jijini Dodoma, kwa kuhakikisha mazingira wezeshi ya biashara yanaimarishwa, Sera na Miongozo rafiki inatekelezwa na fursa zaidi za maendeleo
zinapatikana kwa wanawake wote bila ubaguzi.
Akizungumza na viongozi pamoja na wajumbe wa Jukwaa la
Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Jiji la Dodoma Novemba 28,2025 Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mhandisi. MaryPrisca Mahundi amesema Majukwaa hayo yamekuwa chachu ya mabadiliko katika maisha ya wanawake wa jiji la Dodoma ambapo yameongeza uelewa wa masuala ya fedha, yamewajengea uwezo wa kiuongozi na yamewapa ujasiri wa kuanzisha na kuendeleza shughuli mbalimbali za kiuchumi.
“Majukwaa haya ya wanawake yana umuhimu mkubwa katika ustawi na maendeleo ya wanawake na yameanzishwa ili kutoa fursa kwa wanawake kuweza kukutana, kuchochea ubunifu na ushirikiano, kupitia mafunzo, midahalo na kubadilishana uzoefu
kati ya wanawake wa maeneo mbalimbali.” amesema Naibu Waziri Maryprisca
Vilevile amesema majukwaa hayo yanawapa nafasi ya kujengeana uwezo katika nyanja nyingine za maisha ikiwemo
kuendeleza Tunu za Taifa, Uraia, uzalendo na kutokomeza
vitendo vya Ukatili wa kijinsia.
Aidha Naibu Waziri Maryprisca ameongeza kuwa pamoja na mafanikio na umuhimu wa majukwaa haya kwa wanawake ni
wazi kuwa bado kuna kazi ya kufanya ikiwa ni kuongeza ushirikiano kati ya Sekta Binafsi, Taasisi za kifedha, Serikali na wadau wote ili kuhakikisha wanawake wanaendelea kupata elimu ya kibiashara, fursa za masoko, teknolojia bora, na upatikanaji wa mitaji rafiki.
“Napenda kuwahakikishia kuwa jitihada hizi za kuwezesha majukwaa si tu zinawanufaisha wanawake peke yao, bali zinaimarisha familia, jamii na Uchumi wa Taifa kwa ujumla.” amesisitiza Naibu Waziri

