Mfanyakazi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya, Dkt. Ekaristo Mwang’ande, ametunukiwa tuzo kubwa na sifa za kipekee kwa kuwa mwanafunzi bora wa Shahada ya Uzamili ya Udaktari Bingwa wa mpangilio wa meno, mataya na Uso (Master of Dentistry in Orthodontics and Dentofacial Orthopedics), kwenye mahafali yake ya 19 ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) jijini Da es Salaam.
Akiwapongeza wanafunzi waliofanya vizuri wakati wa sherehe maalum iliyofanyika jijini Dar es Salaam Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Prof. David Mwakyusa amewapongeza wanafunzi waliofanya vizuri katika fani mbalimbali ya afya na kuelezea kuwa mafanikio ya Dkt. Ekaristo ni ushahidi wa juhudi, uzalendo, na ari ya kujifunza waliyonayo, na pia ni mfano wa kuigwa kwa wanafunzi na wafanyakazi wa sekta ya afya nchini.
Nae Dkt. Ekaristo akizungumza baada ya kupokea zawadi na cheti cha heshima, alieleza kuwa, mafanikio haya yametokana na ushirikiano wa karibu alioupata kutoka kwa wanafunzi wenzake, Uongozi wa chuo na wa hospitali pamoja na wafanyakazi wenzake, na familia yake. Alisema, “Hii ni mafanikio ya pamoja, na ninawashukuru wote walionipa ushirikiano na kuunga mkono ndoto zangu za kitaaluma. Ninawaomba wanafunzi wa sekta ya afya wasikate tamaa, bali waendelee kujituma na kuamini kuwa mafanikio ni ya watu wanaojitahidi kwa bidii”
Nae, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya, Dkt. Godlove Mbwanji, na Wafanyakazi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya, wamempongeza Dkt. Ekaristo kwa kutimiza malengo yake na kuonyesha mfano wa kazi nzuri. Wamesema kuwa, mafanikio yake ni motisha kwa wafanyakazi.
Dkt. Ekaristo Mwang’ande amewahi pia kuwa mfanyakazi bora wa mwaka 2021 wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya anatarajiwa kuwa mfano wa kuigwa na wengine katika kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii.

