Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Uyole, Mhe. Dkt. Tulia Ackson, ameanza zoezi maalum la kuwafikia kaya zenye uhitaji zaidi katika Jimbo la Uyole ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mhe. Dkt. Tulia amesema kuwa mwezi wa Desemba umechaguliwa mahsusi kwa ajili ya kuwafikia wananchi walio katika uhitaji mkubwa zaidi, akibainisha kuwa ingawa wahitaji ni wengi katika jamii, lengo ni kuanza na wale walio katika mazingira magumu zaidi.
Amesema kwa siku ya kwanza ya zoezi hilo, wamefanikiwa kufikia kata sita, ambapo kaya 56 zimepatiwa msaada wa chakula pamoja na fedha kidogo kwa ajili ya kununua mboga katika kipindi cha sikukuu. Ameongeza kuwa zoezi hilo litaendelea kwa siku zinazofuata ili kuwafikia walengwa wengine.
Kwa mujibu wa Mhe. Dkt. Tulia, mpango wa jumla ni kufikia kata zote 13 za Jimbo la Uyole, huku jumla ya kaya 130 zikitarajiwa kunufaika na msaada huo.

Aidha, ametoa wito kwa wananchi kuwa na utamaduni wa kuwajali majirani zao, hasa katika kipindi cha sikukuu, kwa kuangalia kama kuna anayehitaji msaada na kumsaidia kulingana na uwezo wao, ili kila mmoja aweze kutabasamu.
Katika hatua nyingine, Mhe. Dkt. Tulia amewashukuru wadau mbalimbali wanaoungana na juhudi hizo, akitaja kupata msaada kutoka kwa mdau mmoja aliyefahamika kwa jina la B2K, ambaye anatokea mkoani Iringa, aliyekutana nao kwa bahati wakati wa utekelezaji wa zoezi hilo katika Kata ya Iganzo, eneo la Asalemba.

Amesisitiza kuwa lengo la zoezi hilo ni “kutabasamisha jamii”, huku akitoa wito kwa wadau na wananchi wengine kuungana nao katika kusaidia wenye uhitaji ili kuimarisha mshikamano na upendo ndani ya jamii.


