Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa (MNEC), Ndele Mwaselela, amewataka waandishi wa habari kuendelea kuzingatia maadili ya taaluma, kuandika habari za maendeleo na kuwasaidia wananchi kwa kuwaseemea, akisisitiza kuwa jamii inawategemea sana waandishi wa habari katika kusikika kwa sauti yao.
Mwaselela ameyasema hayo wakati alipofanya ziara ya kushtukiza katika Ofisi za Waandishi wa Habari Mkoa wa Mbeya (Mbeya Press Club), ambapo alizungumza na baadhi ya waandishi wa habari aliowakuta wakiendelea na majukumu yao ya kila siku ofisini hapo.
Akizungumza katika mazungumzo hayo ya ana kwa ana, Mwaselela alisema kuwa waandishi wa habari wana nafasi ya kipekee ya kuwa daraja kati ya Serikali na wananchi, kwa kuibua changamoto, mawazo na mahitaji ya wananchi kwa uwazi, usahihi na kwa kuzingatia misingi ya maadili ya uandishi wa habari.
“Wananchi wanawategemea sana waandishi wa habari kuwasaidia kuwasemea. Ni muhimu mkaandika habari zinazolenga kusaidia jamii, kuibua changamoto kwa njia ya kitaalamu na kuepuka uandishi wa habari unaochochea migogoro,” alisema Mwaselela.
Aliongeza kuwa pamoja na kuandika habari za maendeleo, waandishi wa habari wanapaswa kuepuka upendeleo wa aina yoyote, akisema kuwa uandishi usiozingatia misingi ya taaluma unaweza kuleta mpasuko na kutoelewana kati ya Serikali na wananchi.
Mwaselela aliwataka waandishi hao kuacha kuandika habari chonganishi, akibainisha kuwa vyombo vya habari vina wajibu mkubwa wa kulinda amani, mshikamano na umoja wa taifa, huku vikichangia maendeleo kupitia uandishi wenye ukweli, uwajibikaji na uzalendo.
Aidha, alieleza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta tofauti, hivyo ni jukumu la vyombo vya habari kuhabarisha jamii kuhusu jitihada hizo sambamba na kutoa nafasi kwa wananchi kueleza changamoto zao kwa njia yenye kujenga.
Kwa upande wake, Mwaselela ambaye pia ni mmiliki wa Shule za Sekondari za Patrick Mission na Paradise Mission, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya viongozi, vyombo vya habari na wananchi ili kuhakikisha maendeleo endelevu yanapatikana.
Ziara hiyo ya kushtukiza ilihitimishwa kwa mazungumzo ya kirafiki na ya kujenga kati ya Mwaselela na waandishi wa habari aliowakuta ofisini hapo, ambapo walibadilishana mawazo kuhusu changamoto za uandishi wa habari na nafasi ya vyombo vya habari katika kuijenga jamii yenye amani na maendeleo.


