Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi, ametembelea Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru mkoani Arusha na kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa chuoni hapo, ikiwemo ujenzi wa jengo la Utawala, kituo cha uhifadhi wa machapisho yanayohusu wanawake, mabweni ya wanafunzi pamoja na Kituo cha Ubunifu wa Kidigitali na Huduma Tandaa (JODIC).
Akizungumza mara baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa jengo la Utawala, Mhe. Mahundi amesema serikali imeendelea kuwekeza katika miundombinu ya vyuo vya maendeleo ya jamii ili kuimarisha mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia, sambamba na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma.
“Miradi inayoletwa hapa chuoni inapaswa kusimamiwa kwa viwango vinavyokubalika ili thamani ya fedha itumike ipasavyo na kwa ubora unaostahili kwa manufaa ya wanafunzi na taasisi kwa ujumla,” amesema Mhe. Mahundi.
Aidha , Mhe. Mahundi amepata fursa ya kuzungumza na wanafunzi wa taasisi hiyo ambapo amewahimiza kutumia elimu wanayoipata chuoni hapo kwenda kuitumikia jamii kwa vitendo kwa kuwa elimu ya maendeleo ya jamii inapaswa kuwa chachu ya mabadiliko chanya katika jamii na siyo kubaki darasani pekee.
Kwa upande wake, Mkuu wa Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru, Dkt. Bakari George, ameishukuru serikali kwa kuendelea kuiunga mkono taasisi hiyo kupitia utekelezaji wa miradi ya kimkakati inayolenga kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.
“Hili jengo la Utawala na miradi mingine inaongeza ufanisi wa kiutendaji na kuboresha huduma kwa wanafunzi, Uwekezaji huu unaofanywa na serikali ni kielelezo cha dhamira yake ya kuimarisha elimu ya maendeleo ya jamii nchini,” amesema Dkt. George.

Ziara hiyo ya Naibu Waziri Mahundi katika Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru imekuwa sehemu ya juhudi za serikali katika kuimarisha elimu ya maendeleo ya jamii nchini, kwa lengo la kuhakikisha vyuo vinaendelea kuzalisha wataalamu wenye ujuzi, ubunifu na maadili watakaotumia elimu yao kutatua changamoto za kijamii, kuendeleza ustawi wa wananchi na kuchangia maendeleo endelevu ya Taifa.
Na Jackline Minja – MJJWMM Arusha

