Katibu Tawala wa Wilaya ya Mbeya, Mohamed Fakii, ametoa onyo dhidi ya uharibifu wa vyanzo vya maji unaotokana na ukataji miti ovyo na kilimo karibu na vyanzo vya maji.
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa Chanzo cha Maji cha Mbawe, kijiji cha Mbawe, Fakii alisema kuwa shughuli za kibinadamu zinaendelea kuhatarisha uendelevu wa vyanzo vya maji licha ya kuwepo kwa maji kwa sasa kutokana na mvua. Alisisitiza kuwa ni marufuku kufanya shughuli zozote ndani ya mita 60 kutoka chanzo cha maji.
Aliwaagiza wananchi wote wanaolima au kufanya shughuli karibu na vyanzo hivyo kuondoka mara moja, huku akizitaka serikali za vijiji na kata kushirikiana kikamilifu katika ulinzi wa vyanzo vya maji na kutoa elimu kwa wananchi.
Ziara hiyo ilifanywa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Mbeya akimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Mheshimiwa Solomon Itunda, akiwa ameambatana na Kamati ya Usalama ya Wilaya.

