ZAIDI ya kaya 200 zimepata madhara ya kukosa makazi baada ya nyumba zao kuezuliwa na nyingine kubomoka kufuatia mvua kubwa zilizoambatana na upepo mkali zinazoendelea kunyesha katika Nyanda za Juu Kusini.
Mbali na makazi kuharibika, vyakula na mavazi pia vimeathirika baada ya maji kujaa kwenye nyumba na mali nyingi kufunikwa na tope.
Uharibifu huo umeripotiwa katika kata sita, ambazo ni Iganzo, Isanga, Karobe, Iyunga, Nzovwe na Iwambi, wakati wa ziara ya Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, Patrick Mwalunenge, aliyefika kujionea hali halisi ya wananchi walioathirika.
Baadhi ya wakazi wamesema chanzo kikubwa cha mafuriko hayo ni mifereji kuziba, hali iliyosababisha maji kuingia moja kwa moja kwenye makazi yao.
Licha ya uharibifu mkubwa wa mali na makazi, hakuna madhara ya kibinadamu yaliyoripotiwa hadi sasa.

