Serikali na TNCC Kuunganisha Mifumo Kidigitali, TRA Yaimarisha Ukusanyaji Mapato
Mbeya-Katika hatua kubwa ya mapinduzi ya kidigitali, Serikali iko katika hatua za mwisho kukamilisha zoezi la kuunganisha mifumo yake ili iweze kusomana na kubadilishana taarifa kwa ufanisi nchi nzima.
Hatua hiyo inalenga kuimarisha mazingira ya biashara kupitia maboresho ya teknolojia na kupunguza urasimu katika utoaji wa huduma.
Kuunga mkono mageuzi hayo, Chemba ya Taifa ya Biashara Tanzania (TNCC) imezindua mafunzo ya wiki moja mkoani Mbeya kuhusu matumizi ya mfumo mpya wa utoaji wa Vyeti vya Usaili (Certificate of Origin) kupitia Tanzania Chamber Portal (TCP).
Mafunzo hayo yanahusisha mikoa 14 ikiwemo Ruvuma, Morogoro na Dodoma, yakilenga kuwajengea uwezo viongozi wa TNCC pamoja na wafanyabiashara ili waweze kutumia mfumo huo kwa ufanisi.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa katika ufunguzi wa mafunzo hayo, mfumo huo utaongeza uwazi, kupunguza urasimu na kuharakisha utoaji wa huduma kwa wafanyabiashara, huku ukiunganisha moja kwa moja mifumo ya TNCC na Serikali kwa ufanisi zaidi.
Kwa upande wake, Afisa forodha Tunduma wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Gwakisa Mwaikenda, alisema mfumo huo shirikishi utaimarisha ukusanyaji wa mapato na kuziba mianya ya upotevu wa mapato kupitia ufuatiliaji wa kidigitali.
Naye Mwenyekiti wa TNCC Mkoa wa Mbeya, Bw. Erick Sichinga, alisema wafanyabiashara wa mkoa huo watanufaika kwa kiasi kikubwa kupitia mfumo huo mpya.
“Kwa wafanyabiashara wa Mkoa wa Mbeya, mfumo huu utapunguza gharama na muda wa kufuatilia Vyeti vya Usaili, hasa kwa wanaojihusisha na biashara za mipakani na masoko ya nje. Kupitia mfumo huu wa kidigitali, tutakuwa na uhakika wa ushindani bora zaidi kikanda na kimataifa, huku tukiongeza ufanisi na uwazi katika shughuli za biashara.”
Warsha hiyo inaratibiwa na TNCC kwa udhamini wa TradeMark Africa kwa kushirikiana na Serikali kupitia TRA, ikiwa ni sehemu ya mkakati mpana wa kuifanya Tanzania kuwa na mifumo ya kisasa, jumuishi na rafiki kwa biashara za kikanda na kimataifa.

