Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Uyole, Dkt. Tulia Ackson, ameunga mkono juhudi za wananchi wa Mtaa wa Bombambili, Kata ya Mwakibete mkoani Mbeya, kwa kuchangia mifuko 100 ya saruji na tripu 10 za mawe kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya zege iliyoanzishwa na wananchi kwa nguvu zao.
Kwa mujibu wa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, vipande viwili vya barabara inayounganisha Kata za Iyela, Mwakibete na Mwasanga vinatarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi milioni 41, ambapo kipande kimoja kimegharimu zaidi ya milioni 23 na cha pili kinakadiriwa kugharimu zaidi ya milioni 18.
Diwani wa Kata ya Mwakibete, Lucas Mwampiki, alimshukuru Dkt. Tulia kwa kuendelea kuunga mkono maendeleo ya kata hiyo, huku akitaja pia msaada wake katika ujenzi wa nyumba inayotarajiwa kukabidhiwa Machi 7, 2026 katika Mtaa wa Itongo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Bombambili, Saidi George Kumbemba, alimpongeza Dkt. Tulia kwa kusaidia wananchi na wadau wanaojitolea kujenga barabara hiyo inayoelekea Makaburi ya Iyela, pamoja na kuendelea kuwatetea katika maendeleo ya miundombinu ya barabara.

