Mbunge wa Jimbo la Mbarali mkoani Mbeya, Bahati Ndingo, amesema maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ni fursa ya kutathmini hatua zilizopigwa katika kuimarisha usawa wa kijinsia na kuhamasisha jamii kuendelea kuwapa wanawake na wasichana nafasi ya kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.
Akizungumza Machi 6, 2026 katika maadhimisho ya siku hiyo yaliyofanyika kiwilaya katika Kata ya Igurusi, Ndingo alisema Tanzania imepiga hatua kubwa kwa kumpa mwanamke nafasi ya juu ya uongozi nchini, akimtaja Rais Samia Suluhu Hassan kama mfano wa mafanikio ya wanawake katika uongozi.
Aidha, alisisitiza kuwa maadhimisho hayo hayalengi kujisifia bali kutambua mchango wa wanaume na wanawake katika kubadilisha mtazamo wa jamii kuhusu uwezo wa mtoto wa kike. Aliongeza kuwa mtoto wa kike ana uwezo wa kufanya kazi na majukumu yoyote kama ilivyo kwa mwanaume.
Maadhimisho hayo ni sehemu ya maandalizi ya kilele cha Siku ya Wanawake Duniani kinachoadhimishwa kila mwaka Machi 8.

