Mashindano ya Riadha ya Betika Mbeya Tulia Marathon yametamatika leo kwa mafanikio makubwa katika Uwanja wa Sokoine, Mbeya Mjini, yakiwashirikisha wanariadha zaidi ya 2,000 kutoka ndani na nje ya Tanzania. Washiriki hao walichuana katika mbio fupi (za ndani ya uwanja) na mbio ndefu (Full Marathon), huku wakionesha viwango vya juu vya ushindani na nidhamu ya hali ya juu.
Mgeni rasmi wa mashindano hayo alikuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko, ambaye aliipongeza Taasisi ya Tulia Trust, chini ya uongozi mahiri wa Mkurugenzi wake ambaye pia ni Mbunge wa Mbeya Mjini, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa IPU, Mhe. Dkt. Tulia Ackson, kwa kufanikisha kwa kiwango cha juu mashindano hayo.
Dkt. Biteko amesema kuwa mashindano hayo si tu yanakuza vipaji vya michezo bali pia ni kichocheo kikubwa cha maendeleo ya kijamii, hasa katika sekta za elimu na afya kupitia mchango wa Tulia Trust.
Kaulimbiu ya mwaka huu, “Mbeya Tulia Marathon 2025: Tunaboresha Miundombinu ya Elimu na Afya”, imeendelea kuonyesha dhamira ya kweli ya Spika Dkt. Tulia Ackson katika kuleta maendeleo ya watu kupitia michezo na taasisi yake ya Tulia Trust.
Tunampongeza kwa dhati Mhe. Spika Dkt. Tulia Ackson kwa uongozi wake wa mfano, uzalendo usioyumba, na moyo wake wa kujitolea kwa ajili ya jamii. Ameendelea kuwa mfano wa kuigwa katika kuchangia maendeleo ya nchi kwa vitendo, na juhudi zake kupitia Mbeya Tulia Marathon zinaendelea kugusa maisha ya Watanzania wengi.