Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) amesema kuwa Wizara inaendelea kushirikiana kwa karibu na Jeshi la Polisi katika kukabiliana na vitendo vya utapeli mtandaoni, hasa vinavyofanyika kupitia huduma za simu na miamala ya kifedha (SimBanking).
Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mheshimiwa Fakharia Shomari Khamisi (Mb.), katika kikao cha Bunge kilichofanyika jijini Dodoma, Mhandisi Mahundi alisema ongezeko la matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) limeleta manufaa makubwa kwa taifa katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kisiasa, huku pia likizua changamoto mbalimbali ikiwemo uhalifu wa mtandaoni.
Kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
(TCRA) kwa robo ya tatu ya mwaka huu wa fedha, idadi ya laini za simu imefikia milioni 90.4, huku watumiaji wa intaneti wakifikia milioni 49.3.
Mhandisi Mahundi alisema mafanikio hayo yameambatana na ongezeko la visa vya utapeli, ambavyo vimekuwa vikiwahadaa wananchi na kusababisha wapoteze fedha zao.
“Serikali kwa kushirikiana na wadau wa mawasiliano imeendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu usalama wa mitandao kupitia kampeni mbalimbali kama vile SITAPELIKI na
NI RAHISI SANA, ili kuongeza uelewa wa wananchi juu ya matumizi salama ya huduma za kidijitali, hususan katika huduma za kifedha,” alisema Mahundi.
Aidha, alisema Serikali kupitia Jeshi la Polisi inaendelea kuimarisha mikakati ya kukabiliana na aina hiyo ya uhalifu na tayari hatua mbalimbali zimechukuliwa dhidi ya wahusika.
Akijibu swali la nyongeza la Mbunge huyo, Mhandisi Mahundi alibainisha kuwa sababu mojawapo inayochochea kuendelea kwa utapeli ni baadhi ya wananchi kushirikiana bila kujua na matapeli kwa kujibu au kufuata maelekezo kutoka kwa ujumbe au simu za kitapeli.
Alitoa wito kwa wananchi kuwa waangalifu na kutotoa ushirikiano kwa mawasiliano yasiyo rasmi au yenye viashiria vya udanganyifu.