Na Mwandishi Wetu
Agosti 3, 2025 — Wazalishaji wa maudhui mtandaoni wametakiwa kuepuka kuchapisha taarifa zinazoweza kusababisha taharuki au kuchochea machafuko, hususan katika kipindi hiki kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika mwishoni mwa mwaka huu.
Wito huo umetolewa na Meneja wa Kitengo cha Huduma za Utangazaji kutoka TCRA, Mhandisi Andrew Kisaka, alipokuwa akiwasilisha mada katika mkutano wa watoa maudhui mtandaoni ulioandaliwa na Tume Huru ya Uchaguzi (INEC).
Mhandisi Kisaka amesema kuwa kipindi cha uchaguzi huwa na hali ya migawanyiko, mivutano na upotoshaji mkubwa, hivyo ni muhimu mabloga na watoa maudhui wengine kujiepusha kusambaza uvumi, kutangaza kwa umakini, kutopendelea upande wowote na kukemea lugha ya chuki.
“Kama unaona maudhui yanaweza kuleta taharuki ni bora kuachana nayo,” amesema Kisaka.
Ametoa mfano wa machafuko ya uchaguzi yaliyotokea Nigeria mwaka 2011, ambapo watu zaidi ya 800 walipoteza maisha, na Kenya mwaka 2007, ambapo zaidi ya watu 1,000 walifariki huku wengine 600,000 wakikosa makazi.
Ameongeza kuwa vyombo vya habari vinaweza kuwa sehemu ya tatizo endapo vitasambaza uvumi au kuonyesha upendeleo wa kisiasa kwa namna isiyozingatia maadili.
“Uvumi ndiyo chanzo kikuu cha vurugu. Vyombo vya habari vinapaswa kuchunguza uvumi na kutoa taarifa sahihi mapema ili kuzuia machafuko ya kulipiza kisasi,” amesema.
Aidha, Kisaka amewataka mabloga kutochapisha au kurudia vichwa vya habari vyenye lugha ya kichochezi, hata kama kauli hizo zimetolewa na wanasiasa. Amesema lugha ya kudhalilisha inaweza kuchochea ghasia na vitendo vya kikatili.
Pia ametoa angalizo kwa mabloga kuacha matangazo ya moja kwa moja ya kampeni, akieleza kuwa kazi hiyo inapaswa kufanywa na waandishi waandamizi waliobobea katika kuripoti wakati wa migogoro.
“Matangazo ya moja kwa moja ya machafuko yanahitaji uzoefu. ‘One Man Show’ wa bloga hauna nafasi katika mazingira hayo ya shinikizo,” amesema.
Kwa mujibu wa TCRA, mafunzo ya namna ya kuripoti wakati wa maafa na katika mazingira ya uchaguzi ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha uchaguzi wa 2025 unafanyika kwa amani kama ilivyokuwa katika chaguzi zilizopita.