#Aipongeza kwa kuwafungulia barabara wakulima
Dodoma
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Bi. Asia Messos ameipongeza Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa ujenzi wa miundombinu ambayo imeweza kuwasaidia wakulima kusafirisha mazao yao kwa wakati.
Ameyasema hayo mara baada ya kutembelea banda la TARURA kwenye Maonesho ya NaneNane Kitaifa yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.
Amesema kwamba kazi kubwa imefanyika katika maeneo mengi na hivyo wameweza kuwarahisishia wakulima kusafirisha mazao yao kwa wakati na kufikisha kwenye masoko.
“Niwapongeze sana TARURA kwa kazi kubwa mnayoifanya vijijini,sisi ni mashahidi katika maeneo yetu,wakulima wanaweza kusafirisha mazao na bidhaa zao kutoka sehemu moja hadi sehemu nyingine, hiyo ni hatua kubwa kwa serikali”.
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini TARURA inaendelea kutoa Elimu kwa wananchi na wadau mbalimbali wanaotembelea banda la maonesho la Wakala huo katika Viwanja vya Nanenane Nzuguni Dodoma ili kuhakikisha kazi zinazotekelezwa na Wakala zinafahamika kwa wananchi.