Imeelezwa kuwa uuguzi na ukunga ni fani ya wito wa kipekee na inayohitaji si maarifa na ujuzi bali heshima, moyo wa kujitolea, maadili ya juu na upendo kwa binadamu.
Hayo yamesemwa na Samwel Mwangoka Mkuu wa Chuo cha Uuguzi na Ukunga Tukuyu katika mahafali ya 14 ya kuhitimu mafunzo ya Stashahada ya uuguzi na ukunga chuoni hapo na kuwasihi kuzingatia maadili kila mahali watakapokwenda na kuwa mfano wa nidhamu, bidii na uadilifu katika kazi.
“..mtakuwa na jukumu kubwa la kutoa huduma bora za afya kwa wananchi na mtakabiliana na changamoto mbalimbali na zinaendelea kubadilika, kuanzia kushughulikia matatizo ya afya ya umma hadi kutoa huduma kwa watu binafsi, familia na jamii kwa ujumla. Naamini elimu mliyoipata imewaandaa na mtaitumia vyema kukabiliana na changamoto.” – amesema Mkuu wa Chuo Samwel Mwangoka.
Ameeleza kuwa ni muhimu wahitimu hao kuwa na jitihada za kuendelea kuongeza ujuzi na kutumia miongozo ya kutolea huduma za afya bila kusahau kuhudumia kila mgonjwa kwa heshima, huruma na upendo kwani vina mchango mkubwa ya kuleta mabadiliko katika afya ya wagonjwa na jamii kwa ujumla.
“kumbukeni kuwa kujifunza katika afya ni maisha yote kwani, huduma za afya zinaendelea kubadilika kutokana na mabadliko ya tekinolojia, mabadiliko ya magonjwa na ni wajibu wako kujifunza na kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia mpya. Kutumia fursa kujiendeleza kitaaluma, kwa kuwa ni kwa kuendelea kujifunza ndipo utaendelea kutoa huduma bora zaidi.” – alisema Mkuu wa Chuo Samwel Mwangoka
Nae Mgeni Rasmi wa mahafali hayo Ndugu Gabriel Godlove Mwakagenda akimuwakilisha Mhe. Anthony Mwantona Mkurugenzi wa God’s Bridge Development Foundation amepongeza Uongozi wa chuo na kueleza kuwa mafanikio hayo yanathibitisha juhudi na kujituma kwa wahitimu na wafanyakazi wa chuo kwa kuandaa wataalamu wa hali ya juu wanaoweza kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya afya.
“Ninapozungumza leo, nawapongeza sana wahitimu wetu kwa kufanikisha hatua hii muhimu zaidi katika maisha yao. Safari yenu haikuwa rahisi, lakini kwa bidii, uvumilivu, na maono makubwa, mmeweza kufikia malengo yenu. Hii ni ishara kwamba, kwa umoja, juhudi, na maadili mema, tunaweza kuleta maendeleo makubwa katika sekta ya afya hapa nchini.” – alisema Mgeni Rasmi
Amesema “Nawaomba mkiwa wahudumu wa afya, muendelee kueneza upendo, huruma, na heshima katika huduma zenu. Kila mtoa huduma anahusika na maisha ya binadamu, na ni jukumu lenu kuhakikisha mnatoa huduma bora zaidi zinazolingana na maadili ya taaluma hii takatifu. Mtaendelea kuwa nguzo muhimu katika ujenzi wa jamii imara na yenye afya.”
Ameipongeza na kuishukuru Serikali kwa jitihada kubwa zilizofanyika katika kuwekeza katika miundo mbinu na kukamilisha jengo la Bweni ambalo ujenzi wake ulisimama tangu mwaka 2011 lakini katika awamu hii serikali imeleta kiasi cha shilingi 432,332,471.00 zilizokamilisha ujenzi huu na kutatua changamoto ya malazi bora, salama na yenye heshima kwa wanafunzi, haya ni maendeleo makubwa katika chuo hiki.
“Uwekezaji huu ni uthibitisho wa nia ya dhati ya serikali katika kuleta ustawi wa wananchi na kuhakikisha kwamba huduma za msingi zinapatikana kwa urahisi na ubora wa hali ya juu. Maboresho haya yamewezesha chuo chetu kutoa mazingira rafiki kwa wanafunzi na wafanyakazi”.
Wakisoma risala yao Judith Mbano na Daudi Malimi wahitimu wa mwaka wa tatu ngazi ya stashahada wa Chuo cha Uuguzi na Ukunga Tukuyu wameeleza kuwa Katika kipindi cha miaka mitatu, wamepata fursa ya kujifunza masomo ya nadharia na vitendo, wameshiriki katika mafunzo ya vitendo vijijini, hospitalini na maeneo mbalimbali ya kijamii, jambo lililowapa uzoefu wa moja kwa moja na kujiandaa kwa maisha ya kitaaluma.
Idadi ya wanafunzi wa mwaka tatu tunaohitimu mafunzo ya Stashahada ya Uuguzi na Ukunga katika chuo cha Uuguzi na Ukunga Tukuyu ni 63, ikiwa idadi ya wasichana ni 32 na idadi ya wavulana ikiwa ni 31.