Mgombea Ubunge wa Jimbo la Uyole, Dkt. Tulia Ackson, amewaomba wananchi wa Uyole kumpigia kura za kishindo Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025 ili aweze kuwaletea maendeleo ya haraka.
Dkt. Tulia ametoa ombi hilo leo tarehe 22 Septemba, 2025 wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Nsalaga mkoani Mbeya katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Itezi kwa lengo la kunadi sera za CCM kuelekea Uchaguzi mkuu.
Amesema kuwa Jimbo la Uyole linayo mahitaji mengi ya msingi ambayo watu pekee na sahihi wa kuyashughulikia ni Dkt. Samia Suluhu Hassan katika nafasi yake ya Urais ambaye atashirikiana naye akiwa katika nafasi ya Ubunge sambamba na Madiwani wa CCM.
Hali kadhalika, Dkt. Tulia amebainisha kuwa kwa kipindi cha miaka mitano ya kuliongoza Jimbo la Mbeya Mjini lililokuwa na Kata 32 ameweza kufanikisha miradi mbalimbali ya kimaendeleo hivyo endapo atapata dhamana ya kuchaguliwa kuliongoza Jimbo jipya la Uyole lenye Kata 13 itakuwa ni kazi nyepesi zaidi kumaliza changamoto zao zote kwa wakati.