Mgombea Ubunge Jimbo la Uyole kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Tulia Ackson, leo Septemba 23, 2025 amefanya mkutano mkubwa wa hadhara katika viwanja vya Ndugunya (Isoso) vilivyopo Kata ya Mwasanga, Jijini Mbeya.
Katika mkutano huo uliovuta mamia ya wananchi, Dkt. Tulia amenadi sera za Chama Cha Mapinduzi huku akisisitiza mshikamano, mshikikiano na mshirikiano katika utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2025 – 2030.
Amewataka wananchi wa Kata ya Mwasanga na Jimbo zima la Uyole kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi ifikapo Oktoba 29, 2025 kushiriki uchaguzi mkuu kwa kuwapigia kura wagombea wote wa CCM kuanzia ngazi ya Udiwani, Ubunge hadi Urais.
“Tukiwa wamoja, tukipiga kura za kishindo, tutamrudisha madarakani Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ameiletea nchi yetu heshima kubwa duniani na maendeleo makubwa ndani ya miaka minne tu. Nawaomba pia mniamini niliendelee kuwatumikia Jimbo la Uyole, na tusimsahau mgombea wetu wa udiwani Kata ya Mwasanga, Ndugu Bandy Nelson, ili tuwe na safu moja ya ushindi wa kijani,” alisema Dkt. Tulia kwa hamasa kubwa.
Aidha, amewapongeza wananchi wa Uyole kwa mshikamano wao katika kuunga mkono miradi ya maendeleo, akiahidi kusimama imara kuendelea kusukuma maendeleo makubwa zaidi katika jimbo hilo.
Mkutano huo uligeuka kuwa sehemu ya hamasa ya kampeni, huku wananchi wakionesha mapenzi yao kwa CCM kupitia nyimbo za kizalendo, mabango na mapambio yaliyopamba anga la Mwasanga.