Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe imezindua rasmi ujenzi wa Soko la Kisasa la Ndizi litakalogharimu Sh Bilioni 2.8, hatua inayotajwa kuwa mabadiliko makubwa katika sekta ya kilimo na masoko ya mazao wilayani humo.
Akizungumza wakati wa utiaji saini wa mkataba huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Bw. Renatus Mchau, amesema Rungwe imechukua hatua ya kihistoria baada ya wananchi kusubiri kwa muda mrefu soko la uhakika la kuuza zao kuu la ndizi—zao ambalo limekuwa mhimili wa uchumi wa wilaya pamoja na mazao mengine kama kahawa, kakao, parachichi na viazi.
Mchau amesema soko la sasa, hususan la Kiwira, halikuwa na mazingira rafiki, jambo lililosababisha usumbufu kwa wakulima na wafanyabiashara, hasa nyakati za mvua. Kupitia maandalizi ya kitaalamu yaliyofanywa na wataalam wa halmashauri, ikiwemo feasibility study, usanifu (designing), tathmini ya athari za mazingira (EIA) na uchunguzi wa kijiolojia (geotech), Rungwe imefanikiwa kupata zaidi ya Sh Bilioni 1.8 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa awamu ya kwanza.
Ametoa shukrani kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kusikiliza kilio cha wananchi na kutoa maelekezo yaliyowezesha mradi huo kuanza kutekelezwa. Aidha, ameikumbusha kampuni ya Kagwa General Supplies Ltd, iliyopewa jukumu la ujenzi, kutekeleza mkataba kwa umakini, uzalendo na viwango vya juu vya ubora.
Kwa upande wa mkandarasi, Emmanuel Madaffa, Kaimu Mkurugenzi wa Kagwa General Supplies Ltd, ndiye aliyewakilisha kampuni hiyo katika hafla ya utiaji saini. Madaffa amesema watatekeleza mradi kwa weledi na uzalendo, wakiahidi “matokeo makubwa badala ya maneno,” huku wakisisitiza kuwa wanafahamu mazingira ya Rungwe na matarajio ya wananchi.
Ujenzi wa soko hilo unatarajiwa kukamilika ndani ya mwaka huu na mwakani, na linatarajiwa kuwa chachu ya kukuza uchumi wa wakulima na kuongeza thamani ya ndizi kutoka Rungwe kwenda katika mikoa mbalimbali na nchi jirani.



