Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba (Mb) ameipongeza Wakala ya Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) kwa utendaji kazi mzuri katika kuhakikisha nchi inakuwa na akiba ya mafuta ya kutosha.
Ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na Menejimenti ya PBPA leo Desemba 6,2025 jijini Dar es Salaam.
“Nawapongeza kwa kazi nzuri mnayoifanya lakini hakikisheni mnatoa elimu kwa Watanzania kuhusu majukumu yenu na kazi zenu” amesema Mhe. Salome.
Aidha, ametumia nafasi hiyo kuitaka PBPA kuwawezesha Watanzania wazawa kuingia kwenye biashara ya mafuta na kufanya kazi kwa ushirikiano.
“Lazima tupate wawekezaji wa Tanzania, tuwawezeshe waingie kwenye hii biashara ” amesisitiza Mhe. Salome.
Naye, Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA), Bw. Erasto Simon amesema wakala hiyo imefanikiwa kuhakikisha kunakuwa na akiba ya mafuta ya kutosha, uwepo wa takwimu sahihi za kiasi cha mafuta pamoja na kuiwezesha Serikali kupanga ukusanyaji wa mapato.
“Mfumo wa Bulk Procurement System (BPS) umesaidia hata nchi za jirani kuagiza mafuta kwa karibia asilimia 95 sambamba na kudhibiti ubora wa bidhaa za mafuta yanayoingia nchini.
Amefafanua kuwa nchi za jirani kama Malawi, Zambia, Uganda, Rwanda, Zimbabwe na Namibia wanaendelea kutembelea Tanzania na kujifunza kuhusu namna bora ya uagizaji mafuta katika nchi zao.
Amesema PBPA imefanikiwa kuratibu uagizaji wa mafuta kwa ufanisi mkubwa kutokana na uwazi uliopo katika mchakato mzima wa uagizaji mafuta.
Lengo la ziara ya Mhe. Makamba katika ofisi za PBPA ni kujifunza kuhusu majukumu ya PBPA pamoja na kujitambulisha mara baada ya kuteuliwa na Mheshimiwa Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Naibu Waziri katika Wizara ya Nishati.

