Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalum Mhe.Mhandisi Maryprisca Mahundi ametembelea Kituo cha Tumaini la Wazee kilichopo Kata ya Majengo Jijini Mbeya kwa lengo la kuwapa tabasamu na kuwatia moyo kwa kutoa zawadi mbalimbali.
Akiongea na Wazee zaidi ya hamsini wa Kata ya Majengo Mhandisi Maryprisca Mahundi amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan imeweka mkakati mzuri kwa ajili ya kuwasaidia wazee hususani katika huduma za afya.
Kwa upande wake Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Mbeya Salum Manyendi amesema Serikali imedhamiria kuanza kutoa huduma za afya kwa wazee kwa kuwafuata majumbani ili kuwaondolea kadhia ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya katika zahanati, vituo vya afya na hospitali.
Mwenyekiti wa Tumaini la Wazee Moses Sanga mbali ya kushukuru kupokea msaada huo hakusita kubainisha baadhi ya changamoto zinazowakabili wazee zikiwemo za baadhi ya wazee kushindwa kwenda hospitali kutokana na ukata wa fedha unaotokana na kukosa wategemezi.
Kwa sasa Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Makundi Maalum ikiongozwa na Waziri Dkt. Dorothy Gwajima na Naibu wake Mhandisi Maryprisca Mahundi wanafanya ziara nchi nzima kwa lengo la kutoa faraja kwa Makundi mbalimbali wakiwemo wazee na kubaini changamoto zinazowakabili ili Serikali iweze kuzitatua.
Na WMJJWM- Mbeya

