Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi, amewataka watoto waliopo katika Shule ya Maadilisho Irambo mkoani Mbeya kuchukulia uwepo wao chuoni hapo kama fursa ya mabadiliko chanya na maandalizi ya maisha bora ya baadaye.
Akizungumza wakati wa ziara yake shuleni hapo, Mhe. Mahundi alisema watoto hao hawapaswi kujiona tofauti au waliopotea, bali wajione kama vijana wanaojengwa upya ili kuwa raia wema na viongozi wa kesho.
“Kuwepo kwenu hapa siyo adhabu bali ni mpango wa Mwenyezi Mungu wa kuwajenga upya. Maadilisho ni mabadiliko ya kweli, na kesho yenu bado ni njema,” alisema Mhe. Mahundi.
Amefafanua kuwa Shule ya Maadilisho siyo gereza, bali ni kituo cha malezi na elimu kwa watoto walio chini ya miaka 18 waliokiuka sheria, kwa lengo la kuwarekebisha kimaadili, kielimu na kitabia ili warejee salama kwenye jamii.
Mhe. Mahundi alisema Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum ina wajibu wa kisheria na kiserikali kuhakikisha mtoto analindwa, anakuzwa, analelewa na kuandaliwa kuwa raia mwema wa Taifa.
Aidha, aliwahimiza watoto hao kutumia vyema fursa ya elimu inayotolewa shuleni hapo ikiwemo elimu ya msingi na sekondari, akisisitiza kuwa wapo watoto waliopita katika shule hiyo na baadaye kufanikiwa kielimu hadi vyuo vikuu.
“Msikate tamaa. Wapo waliowahi kuwa hapa, wakasoma, wakafaulu, wakaendelea na masomo hadi vyuo vikuu. Na nyinyi mnaweza,” aliongeza.
Katika hotuba yake, Mhe. Mahundi pia aliwasihi watoto hao kumcha Mungu bila kujali dhehebu lao, kuheshimu wakubwa na wadogo, kuwa watiifu, wasikivu na kuacha kabisa mienendo iliyowapeleka kwenye makosa.
Akiwahakikishia jamii, alisema watoto watakaomaliza muda wao wa maadilisho watarejeshwa kwa wazazi na jamii zao, akitoa wito kwa jamii kuwapokea kwa upendo bila kuwanyanyapaa.
Ziara hiyo ilihitimishwa kwa Mhe. Mahundi kukabidhi zawadi mbalimbali kwa watoto hao, ikiwa ni sehemu ya kuwatia moyo na kuwajengea matumaini mapya ya maisha.



