Mbunge wa Jimbo la Mbeya Vijijini, Mhe. Patali Shida Patali, amesema Serikali imetoa zaidi ya shilingi milioni 250 kwa ajili ya matengenezo ya barabara ya Igyoma–Ilambo (takribani km 9), ambapo mkandarasi tayari ameanza kazi ili kuwezesha wananchi kuendelea na shughuli zao za kiuchumi.
Amesema pia fedha zimetolewa kwa ajili ya ukarabati wa barabara ya Isionje–Kikondo ambayo imekuwa na changamoto kubwa wakati wa mvua, huku mkandarasi akiwa tayari eneo la kazi na hali ya barabara ikionekana kuimarika ikilinganishwa na miaka iliyopita.
Akizungumzia changamoto ya barabara iliyo karibu na Shule ya Maadilisho Irambo, Mhe. Patali amesema hakuna mgogoro bali kuna taratibu za kisheria zinazohitajika kufuatwa baada ya barabara hiyo kuhamishwa kutoka TARURA kwenda TANROADS, na kuomba mamlaka husika kuharakisha mchakato huo kwa manufaa ya wananchi.
Kauli hiyo ilitolewa wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi, katika Shule ya Maadilisho Irambo mkoani Mbeya.

