Child Support Tanzania imeendesha kikao na madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya kupitia Kamati ya Elimu, Afya na Maendeleo ya Jamii kwa lengo la kuimarisha utekelezaji wa Elimu Jumuishi, hususan kwa watoto na watu wenye ulemavu.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa Child Support Tanzania, Bi. Noela Msuya Shawa, amesema kupitia mradi wa Sauti Zetu unaofadhiliwa na Oxfam na kutekelezwa kwa ushirikiano na AkiElimu, madiwani wamepatiwa mafunzo kuhusu Mpango Mkakati wa Taifa wa Elimu Jumuishi, miongozo yake na wajibu wao katika kuhakikisha utekelezaji wake kwa ubora katika shule za kata zao.
Kwa upande wao, madiwani wamesema mafunzo hayo yamewajengea uelewa mpana kuhusu masuala ya watoto na watu wenye ulemavu. Mh. Juma Samson Simbeange, Diwani wa Kata ya Nsoho, amesema atahakikisha masuala ya watoto yanapewa kipaumbele wakati wa kupitisha bajeti za Halmashauri ili kuwasaidia watoto wanaohitaji msaada maalum.
Naye Mh. Clemence James Mwandemba, Diwani wa Kata ya Nsalaga, amesema elimu hiyo itawasaidia viongozi kushiriki kikamilifu katika upangaji wa bajeti kwa kuzingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu, ikiwemo mikopo ya asilimia kumi inayotengwa kwa makundi maalum, pamoja na kuhamasisha jamii kutowaficha watu wenye ulemavu bali kuwapeleka kwenye taasisi zinazotoa msaada na elimu.

Child Support Tanzania imepongeza dhamira ya madiwani na kusisitiza kuwa ushirikiano kati ya taasisi na viongozi wa serikali za mitaa ni muhimu katika kufanikisha elimu jumuishi na kujenga jamii isiyobagua.


