Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya kwa kushirikiana na NHIF Mkoa wa Mbeya wamekutana na kundi la watu wenye ulemavu mkoani Mbeya kutoa elimu kuhusu umuhimu wa kujiunga na Bima ya Afya kwa wote.
Akifungua kikao hicho Februari 25, 2026, Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo Dkt. Godlove Mbwanji alisema lengo ni kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata uelewa wa bima hiyo, kwani ni miongoni mwa makundi maalumu yaliyopewa kipaumbele na Serikali ya Awamu ya Sita katika utekelezaji wa sheria ya Bima ya Afya kwa wote.
Msimamizi wa NHIF mkoa wa Mbeya, Bw. Nicolaus Mwangomo, alieleza kuwa washiriki walipatiwa elimu kuhusu utaratibu wa uchangiaji, faida na dhana ya bima hiyo, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi ya Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya Bima ya Afya kwa wote.
Kwa niaba ya washiriki, Bi. Rebecca Ramadhani alishukuru kwa elimu hiyo akisema itasaidia watu wenye ulemavu kukabiliana na changamoto za matibabu na kuboresha upatikanaji wa huduma za afya.

