Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM Wilaya ya Mbeya Mjini, Emmanuel Mwalupindi, amekabidhi tuzo na vitabu kwa walimu wa Shule ya Sekondari ya Sangu, shule inayomilikiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), ikiwa ni sehemu ya pongezi kwa kufanya vizuri katika matokeo ya Kidato cha Nne mwaka 2025.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi tuzo hizo iliyofanyika shuleni hapo Mbeya Mjini, Mwalupindi amesema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mzuri kati ya walimu, wanafunzi na wazazi, na ni jambo la kujivunia kuona shule ikiendelea kufanya vizuri kitaaluma.
Ameeleza kuwa katika matokeo ya mwaka 2025, shule hiyo haikuwa na mwanafunzi mwenye daraja la sifuri (Division 0) wala daraja la nne (Division IV), hali inayoonesha kiwango kizuri cha ufaulu na nidhamu ya wanafunzi katika masomo.
“Tumeona ni muhimu kuwapongeza walimu na wanafunzi kwa juhudi zao. Kutopata sifuri wala four ni ishara kwamba kuna kazi kubwa imefanyika darasani. Jumuiya ya Wazazi itaendelea kuwekeza katika elimu ili kuongeza ubora zaidi,” amesema.
Aidha, amewahimiza wanafunzi kuendelea kusoma kwa bidii na kujiwekea malengo makubwa, huku akiwataka walimu kuendeleza moyo wa kujituma ili shule iendelee kuwa mfano wa kuigwa miongoni mwa shule za wazazi nchini.
Kwa upande wake, uongozi wa shule umeishukuru Jumuiya ya Wazazi kwa mchango wa vitabu, tuzo pamoja na huduma ya futari, ukieleza kuwa msaada huo utaongeza ufanisi wa ujifunzaji na kuimarisha zaidi matokeo ya mitihani ijayo.


