Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mbeya na Mbunge, Patrick Mwalunenge, amepongeza juhudi za Jumuiya ya Wanawake wa Mbeya Zonal Referral Hospital (MZRH) kwa kutoa zawadi ya mashine ya kisasa ya kupima umeme wa kichwa (EEG) yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 67, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Samia Suluhu Hassan katika kuboresha huduma za afya nchini.
Akizungumza kama Mgeni Rasmi katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika hospitalini hapo, Mwalunenge alisema hatua ya wanawake hao ni mfano wa uzalendo na mshikamano katika kuunga mkono maendeleo ya sekta ya afya.
Amesema mchango huo unaonyesha namna ambavyo makundi ya kijamii yanaweza kushiriki moja kwa moja katika kuimarisha huduma za matibabu na kusaidia wananchi kupata huduma bora zaidi.
Katika kuunga mkono juhudi za umoja huo, Mwalunenge alichangia shilingi milioni 3 taslimu kwa ajili ya kuendeleza shughuli na miradi ya maendeleo ya jumuiya hiyo, huku akiahidi kuendelea kutoa ushirikiano wa hali na mali pale utakapohitajika.
Mashine hiyo ya EEG inatarajiwa kuboresha huduma za utambuzi wa magonjwa ya mfumo wa fahamu kwa wananchi wa kanda ya Nyanda za Juu Kusini na kupunguza changamoto ya wagonjwa kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hiyo.

