Sheikh Ibrahim Bombo amempongeza Mbunge wa Jimbo la Uyole na Rais wa Inter‑Parliamentary Union (IPU) Tulia Ackson kwa kuandaa futari iliyowakutanisha wananchi mbalimbali nyumbani kwake.
Akizungumza wakati wa futari hiyo, Sheikh Bombo alimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwakutanisha watu wa makundi tofauti na kueleza kuwa kitendo cha kuwakaribisha wananchi kufuturu pamoja ni ishara ya moyo wa kujitolea na kuwajali wananchi.
Alisema watu waliopata futari hiyo wakiwemo wazee, wanawake, watoto na viongozi wa dini wanapoendelea kusema “Alhamdulillah”, baraka zake humrudia pia aliyeandaa futari hiyo.
Sheikh Bombo alimuombea Tulia Ackson aendelee kupewa nguvu, afya na ulinzi ili kuendelea kuwahudumia wananchi, huku akiwataka viongozi wengine kuiga moyo wa ukarimu na huduma kwa jamii.

