Author: Mbeya Yetu

Tarehe 27.11.2024 saa 12:30 jioni eneo la Mbembela Jijini Mbeya katika
barabara kuu ya Mbeya – Tunduma, Gari lori namba T.537 DNC na Tela
namba T.241 ARG aina FAW iliyokuwa imepakia madini ya Sulphur ikitokea
Dar es Salaam kuelekea Tunduma Mkoa wa Songwe ilipoteza uelekeo na
kugonga magari sita, bajaji nne, Pikipiki moja na kusababisha vifo vya watu
watatu, wawili papo hapo na mmoja amefariki dunia leo Novemba 28, 2024
akiwa anaendelea na matibabu.
Magari yaliyohusika katika ajali hiyo ni T.199 DYF Toyota Coaster, SU 44682
Toyota Double Cabin mali ya Shirika la Posta Mbeya iliyokuwa ikiendeshwa na
Fredy Mwasanga [48] mkazi wa Soweto, Gari T.134 DXK Toyota Double Cabin
iliyokuwa ikiendeshwa na Lusekelo Mwaseba [48] mkazi wa Sae, Gari T.370
ABN Toyota Land Cruiser, Gari T.344 BTS Toyota Cresta na Gari T.474
EHL/t.449 EHL aina ya FAW iliyokuwa ikiendeshwa na Alon Ruben [50] mkazi
wa Isanga.
Aidha, katika ajali hiyo Bajaji nne ziligongwa ambazo ni MC.446 DYK, MC.649
DWL, MC.138 DKC na MC.261 EBN na Pikipiki moja ambayo haijafahamika
namba zake za usajili. Waliofariki katika ajali hiyo bado hawajatambulika,
wawili jinsia ya kiume na mmoja jinsia ya kike. Majeruhi tisa wanaendelea na
matibabu katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya.
Chanzo cha ajali ni uzembe wa Dereva kushindwa kulimudu Gari kwenye
eneo lenye mteremko. Jitihada za kumtafuta Dereva kwa kushirikiana na
mmiliki wa Gari zinaendelea.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea kutoa wito kwa madereva kuwa
makini na kufuata sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazoweza
kuepukika.
Imetolewa na:
Benjamin Kuzaga – SACP
Kamanda wa Polisi,
Mkoa wa Mbeya.

Read More

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson, amesema kifo cha Mbunge wa Kigamboni na Mkurugenzi Mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, Dkt. Faustine Ndugulile, kimeacha simanzi kubwa kwa Bunge na Watanzania kwa ujumla kutokana na mchango wake mkubwa katika maendeleo ya taifa.

Akizungumza mara baada ya kupiga kura katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Mtaa wa Uzunguni A, Jijini Mbeya leo tarehe 27 Novemba, 2024, Dkt. Tulia amesema kuwa nyota ya Dkt. Ndugulile imezimika wakati akiwa ameanza kung’ara katika anga za kimataifa. Alikuwa aanze rasmi majukumu yake mapya ya kimataifa mwezi Machi mwaka 2025.

Dkt. Tulia amesema kuwa Bunge limepoteza Mbunge mahiri ambaye pia alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI. Mchango wake uliwezesha kufanikisha mabadiliko makubwa ya sheria na sera katika sekta za afya na mapambano dhidi ya UKIMWI.

Aidha, amewataka Wananchi wa Kigamboni kuwa wavumilivu katika kipindi hiki ambacho wamempoteza Mbunge wao na kumuombea apumzike kwa amani.

Dkt. Ndugulile amefarikidunia usiku wa kuamkia leo nchini India alipokuwa akipatiwa matibabu.

Read More

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa wawili ambao ni Ramadhan Tembo Mwakilasa [28] na Mariamu Charles Mwashambwa [28] wote wakazi wa TEKU viwandani Jijini Mbeya kwa tuhuma za mauaji ya mtoto Chloy Ramadhan [04] kwa kumpiga fimbo sehemu mbalimbali za mwili.

Ni kwamba Novemba 25, 2024 saa 2:00 usiku huko Mtaa wa TEKU viwandani Jijini Mbeya, mtoto Chloy Ramadhan [04] alifariki dunia baada ya kupigwa fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake na baba yake mzazi aitwaye Ramadhan Tembo Mwakilasa [28] akishirikiana na mama yake wa kambo aitwaye Mariamu Charles Mwashambwa [28] wote wakazi wa TEKU viwandani.

Uchunguzi umebaini kuwa chanzo cha tukio hilo ni ukatili na unyanyasaji kwa kumuadhibu mtoto baada ya kujisaidia kwenye nguo alizokuwa amezivaa.

Jeshi la Polisi linawataka wazazi/walezi kuacha vitendo vya kujichukulia sheria mkononi dhidi ya watoto pindi wanapokosea na badala yake watumie njia sahihi na salama kuwafundisha au kuwaelekeza bila kusababisha madhara.

Read More