Shule ya awali na msingi Holy Land ya Makongolosi Chunya Mkoani Mbeya inayonilikiwa na Lawena Nsonda(Baba Mzazi)imefanya mahafali ya kwanza ya darasa la Saba tangu kuanzishwa kwake miaka saba iliyopita mgeni rasmi akiwa ni Titho Tweve.
Katika hotuba yake Titho Tweve amewataka wazazi kuwekeza kwenye elimu ili watoto wawe na maisha bora.Aidha Tweve amechangia tani tano za saruji zenye thamani ya shilingi milioni tano kwa ajili ya ujenzi wa uzio kuimarisha usalama wa watoto.
Tweve ameupongeza uongozi wa shule ya Holly Land Pre and Primary School kwa namna ilivyojikita kutoa elimu bora hali iliyowafanya wazazi kutoka maeneo mbalimbali nchini kuwaleta watoto shuleni hapo.
Awali Mwalimu Mkuu wa shule ya Holly Land Yona Mwakalinga amesoma taarifa ikionesha mafanikio tangu kuanzishwa ambapo ilianza na watoto wawili lakini kwa sasa ina watoto zaidi ya mia sita.
Mwakalinga amesema shule imekuwa na muendelezo mzuri wa matokeo ya darasa la nne Kiwilaya,Kimkoa na Kitaifa ambapo matokeo ya mwaka 2021 mtihani wa darasa la nne Kitaifa shule ya Holly Land iliongoza.
Mkurugenzi wa Holy Land Lawena Nsonda amesema ushirikiano uliopo baina yake,walimu, watumishi na wanafunzi ndiyo siri ya mafanikio.
Pia malipo ya mishahara kwa wakati na motisha mbalimbali umefanya watu wote kufanya kazi kwa bidii hivyo kuongeza ufaulu wa wanafunzi na matarajio ni kufanya vizuri zaidi mtihani wa darasa la Saba.
Lawena Nsonda ameahidi wanafunzi wanaohitimu mwaka huu wakiongoza Kitaifa atawapeleka Dubai kwa ajili ya mapumziko.
Lawena Nsonda amesema awali wanafunzi walioongoza mtihani wa darasa la nne aliwapeleka mapumziko Jijini Dar es Salaam na Zanzibar kwa usafiri wa ndege.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa shule ya Holly Land ambaye ni mke wa Lawena Nsonda,Winfrida Lawena amesema mumewe ni mlezi wa watoto hivyo inafanya kutekeleza kila huduma kwa watoto hali iliyowafanya wazazi kupenda kuwaleta watoto na watoto kupenda masomo.
“Baadhi ya watoto shule ikifunga wengi wao hawapendi kwenda nyumbani kutokana na malezi bora ya watoto kutoka kwa walimu”alisema mke wa Lawena.
Wadau mbalimbali waliohudhiria mahafali hiyo wamemuunga mkono kwa kuchangia fedha ili kukamilisha wa uzio.