Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Mhe. Dkt. Tulia Ackson, amehudhuria hafla ya kuadhimisha miaka 135 ya Bunge la Hungary, maadhimisho ambayo yameambatana na kuanzishwa kwa Umoja wa Mabunge Duniani. Hafla hii imefanyika tarehe 8 Oktoba, 2024 katika Ukumbi wa Bunge la Hungary Jijini Budapest.
Katika hotuba yake, Dkt. Tulia ameipongeza Hungary kwa hatua thabiti waliyochukua miaka 135 iliyopita kwa kuungana na mataifa machache kusimamia sauti za pamoja za mabunge duniani.
Aidha, amehimiza Bunge la Hungary kuendelea kushikilia misingi ya Umoja wa Mabunge Duniani, ikiwa ni pamoja na kukuza demokrasia, kutekeleza malengo ya maendeleo endelevu na kutoa kipaumbele kwa amani na usalama duniani. Pia, amesisitiza umuhimu wa Hungary kudumisha utambulisho wake kama sehemu ya Ulaya ya Kati, bila kubeba sera, haki na tamaduni za mataifa mengine.
Zaidi ya hayo, Dkt. Tulia ameonesha utayari wa IPU kuendelea kushirikiana na Bunge la Hungary huku akiomba taifa hilo kuwa mstari wa mbele katika juhudi za kutafuta amani kwa mataifa jirani yaliyo kwenye migogoro ya kivita.