Wanariadha wa Jeshi la Polisi na Jeshi la Wananchi waliofanya vyema katika mashindano ya Mbio ndefu na fupi katika michuano ya mbio maarufu NAGAI City Marathon 2024 wamepongezwa kwa kuibuka washindi wa kwanza na kupewa medali za dhahabu.
Pongezi hizo zimetolewa na Afisa Mnadhimu wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Debora Lukololo kwa Niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi, wakati wa mapokezi ya wachezaji hao waliowasili Nchini leo Oktoba 18, 2024 kupitia Uwanja wa Kimataifa wa Ndege (KIA).
Mbio hizo zilifanyika jijini Nagai nchini Japan Oktoba 13, 2024 huku Wanamichezo hao wakipeperusha vyema Bendera ya Tanzania katika michuano hiyo ya kimataifa ambapo mataifa kadhaa yalishiriki.
ACP Lukololo amesema wachezaji hao kwa Umoja wao wameendelea kuwa wazalendo kwa kuipambania Tanzania katika medani za Michezo lakini pia kuitangaza Nchi yetu katika sekta ya utalii kupitia mashindano hayo kwa kufanya vyema kwenye nafasi za juu.
Amendelea kusema kuwa Jeshi hilo kwa kushirikiana na wadau wengine wa michezo litaendelea na Mikakati yake ya kuendelea kuwanoa wanamichezo wengine kwa ajili ya kufanya vyema katika mashindano ya ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.
Kwa upande wake kocha wa Timu ya Riadha ya Polisi Sajenti Oswald amesema siri kubwa ya ushindi kwa wanamichezo hao ni kuwa na maandalizi mazuri lakini pia kupata ushirikiano wa karibu na msaada kutoka kwa viongozi wao pindi wanapohitaji.
Naye Konstebo Jumanne Ndege wa Jeshi la Polisi ambaye aliibuka msindi wa kwanza katika mbio za kilometa 21 upande wa wanaume amemshukuru Mungu kwa namna ambavyo amewaongoza kufanya vizuri kuanzia kipindi cha maandalizi hadi wakati wa mashindano.
Katika mishindano hayo Mwanariadha Natalia Elisante alitawazwa kuwa mshindi wa kwanza kwa upande wa wanawake Mbio za masafa yaani kilometa 42 ‘Full Marathon’ huku pia kwa wanaume Charles Sulle akishinda.
Kando na Mbio ndefu kwa upande wa Mbio fupi yaani kilometa 21 Watanzania pia walifanya vyema “Half Marathon’, ambako kwa Wanawake Neema Kisuda alishinda nafasi ya kwanza na Kwa upande wa Wanaume, ilishuhudiwa Jumanne Ndege akiibuka mshindi wa kwanza.
Takwimu inaendelea kuibeba Tanzania katika mishindano hayo ambapo mwaka 2022 na 2023 Tanzania ilifanya vyema katika Mbio hizo kwa kuibuka washindi wa kwanza.