Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) amelishukuru Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kwa kuunga mkono juhudi za Serikali ya Tanzania za kuendeleza uhifadhi kwa kupambana na ujangili na biashara haramu ya nyara pamoja na kuimarisha ustahimilivu wa Bioanuai ya Misitu ya Mazingira Asilia Tanzania dhidi ya athari za mabadiliko ya Tabianchi.
Ameyasema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkazi, wa UNDP, Bw. Shigeki Komatsubara leo Oktoba 22,2024 jijini Dodoma.
“Shirika la UNDP limeendelea kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii katika utekelezaji wa Mradi wa Kupambana na Ujangili na Biashara haramu ya Nyara pamoja na Mradi wa Kuimarisha Ustahimilivu wa Bioanuai ya Misitu ya MazingiraAsilia Tanzania Dhidi ya Athari za Mabadiliko ya Tabianchi ambayo inafadhiliwa na Mfuko wa Mazingira Duniani (GEF) kupitia UNDP kwa jumla yad ola za Marekani 12,191,597” amesema Mhe. Chana.
Naye, Mkurugenzi Mkazi, Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Shigeki Komatsubara alitumia fursa hiyo kuipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa ushirikiano wake inaoutoa katika utekelezaji wa miradi hiyo huku akisisitiza kuwa UNDP iko tayari kuendeleza ushirikiano huo kwa miradi ya sasa na ijayo.
Aidha, Bw. Komatsubara aliipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa tuzo za Kimataifa za World Travel Awards ambazo Tanzania imezipata katika sekta ya Utalii na kuishauri Wizara namna bora ya kushirikiana katika kutumia teknolojia ya kidijitali katika kutangaza utalii.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki, Bw. Deusdedith Bwoyo pamoja na baadhi ya Maafisa Waandamizi kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na Shirika la UNDP.