Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb), amemtaka Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji kushirikiana na mkandarasi anayetekeleza mradi wa maji wa chanzo cha Mto Kiwira kuweka makubaliano maalum na kiwanda kinachotengeneza mabomba yatakayotumika katika zaidi ya kilomita 30 za mradi huo, ili kuhakikisha mabomba yote yanatengenezwa kwa wakati mmoja.
Mhe. Aweso ametoa maelekezo hayo leo alipofanya ziara kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo, ambapo alieleza kuridhishwa na kazi kubwa iliyofanyika chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mbeya (MBEYAUWSA). Hata hivyo, alieleza kuwa changamoto kubwa iliyobainika ni ucheleweshaji wa ulazaji wa mabomba kutoka kwenye chanzo cha maji hadi kwenye tanki kuu — tatizo linalosababishwa na uchelewaji wa upatikanaji wa mabomba katika eneo la mradi.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa MBEYAUWSA, CPA Gilbert Kayange, alisema kuwa mradi huo ni wa kimkakati na utakapokamilika utaongeza upatikanaji wa huduma ya maji kwa wakazi wa Jiji la Mbeya na maeneo jirani kwa kipindi cha zaidi ya miaka 20 ijayo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa MBEYAUWSA, Bi. Edna Mwaigomole, aliipongeza Serikali kwa utayari wake wa kutoa fedha zinazohitajika kukamilisha mradi huo kwa wakati, akisema hatua hiyo inaonesha dhamira ya dhati ya kuwaletea wananchi maendeleo.
Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Beno Malisa, amemuomba Waziri Aweso kuisaidia taasisi ya Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Mbeya kwa kuiwezesha kifedha ili kukamilisha zaidi ya miradi 10 ya maji inayosuasua kutokana na ukosefu wa fedha kwa wakati.


“RUWASA imekuwa ikikumbwa na changamoto ya fedha, jambo ambalo linaathiri kasi ya utekelezaji wa miradi ya maji vijijini. Tunaomba Wizara itazame hili kwa jicho la huruma,” alisisitiza Mhe. Malisa.