Arusha, Agosti 4, 2025
Tanzania imepewa heshima ya kuwa mwenyeji wa Warsha ya Wakuu wa Taasisi za Kuzuia na Kupambana na Rushwa kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), itakayofanyika kwa siku tatu kuanzia Agosti 4 hadi 6, 2025, katika Hoteli ya Gran Melia, jijini Arusha.
Warsha hii ya kimataifa inafanyika wakati Tanzania ikiwa na jukumu la Uenyekiti wa Kamati ya Kupambana na Rushwa ya SADC (SADC Anti-Corruption Committee – SACC) kupitia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), nafasi ambayo ilianza rasmi Oktoba 2, 2024.
Hii ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya nchi wanachama chini ya Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC ambayo kwa sasa inaongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, tangu Agosti 17, 2024.
Warsha hiyo pia itaambatana na maadhimisho ya miaka 20 ya utekelezaji wa Itifaki ya SADC Dhidi ya Rushwa, itifaki ambayo ilianza kutekelezwa rasmi Julai 2005 kwa lengo la kuimarisha mifumo ya kuzuia, kugundua, kuadhibu na kutokomeza rushwa katika sekta za umma na binafsi ndani ya nchi wanachama.
Malengo mahsusi ya warsha hii ni pamoja na:
-
Kutafakari miaka 20 ya utekelezaji wa Itifaki ya SADC Dhidi ya Rushwa – mafanikio na changamoto.
-
Kutathmini mafanikio yaliyopatikana na kubaini mapungufu katika sheria, uwezo wa taasisi na ushirikiano wa kikanda.
-
Kuweka vipaumbele vya kimkakati kwa mustakabali wa mapambano dhidi ya rushwa katika ukanda wa SADC.
Katika warsha hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Bw. Crispin Francis Chalamila, ambaye pia ni Mwenyekiti anayemaliza muda wake wa SACC, atakabidhi rasmi kijiti cha Uenyekiti kwa mwakilishi kutoka nchi ya Malawi.
Ni muhimu kukumbusha kwamba Tanzania ilipongezwa na Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa SADC katika mkutano wao wa 27 uliofanyika Julai 21–25, 2025 jijini Dar es Salaam. Katika mkutano huo, Katibu Mtendaji wa SADC, Elias Magosi, alisifu juhudi za Tanzania katika mapambano dhidi ya rushwa, akieleza kuwa nchi imeonesha mafanikio makubwa katika maeneo ya mifumo ya kisheria, dhamira ya kisiasa na ushiriki wa wadau.
Kupata heshima ya kuwa mwenyeji wa warsha hii ni ushahidi wa nafasi ya Tanzania katika juhudi za kimataifa za kupambana na rushwa, kuimarisha utawala bora, kuendeleza amani na kukuza maendeleo ya kiuchumi katika kanda.
TAKUKURU imesisitiza kuwa imejipanga kuhakikisha kuwa maazimio ya warsha hii yatakuwa na mchango chanya kwa taifa na ukanda wa SADC kwa ujumla.
Mwisho
Imetolewa na: Kitengo cha Mawasiliano – TAKUKURU
Arusha, Tanzania